Waziri wa Leba na ulinzi wa jamii Dkt. Alfred Mutua, amesema kuwa Wakenya 234 wameripotiwa kuwa waathiriwa wa ulanguzi wa binadamu tangu mwaka 2019.
Alipofika mbele ya bunge la Senate leo Jumatano, waziri huyo hata hivyo alisema serikali imewashughulikia vilivyo wakenya hao kupitia kamati ya kukabiliana na ulanguzi wa watu.
“Kamati ya kukabiliana na ulanguzi wa watu ilishughulikia visa vya wakenya wanaofanya kazi ughaibuni na ambao wamedhulimiwa kwa njia moja au nyingine.
Dkt. Mutua alisema waathiriwa hao 234 walirejeshwa hapa nchini kutoka Uturuki, Lebanon, Iraq, Saudi Arabia, Muungano wa Milki za Kiarabu, Jordan, Myanmar, Qatar na Laos.
Wakati huo huo waziri huyo serikali imo mbioni kuwarejesha nyumbani wakenya waliojifungua wakiwa ughaibuni.
Mutua alisema wakenya hao watalazimika kufanyiwa uchunguzi wa DNA mara tu watakaporejea humu nchini ili kuhakikisha watoto hao ni wao katika juhudi za kupunguza visa vya ulanguzi wa watoto.
Kulingana na waziri huyo, idadi kubwa ya wakenya wamejifungulia ughaibuni na kwamba serikali inajaribu kuwarejesha nyumbani pamoja na watoto wao.
Alitoa wito kwa wakenya wanaoelekea ughaibuni kufanya kazi, kujiepusha na mambo ya uanaharakati, akiongeza kuwa watafunzwa kufuata mifumo ya sheria katika nchi husika.