Mutua atakiwa kurejesha milioni 27 alizolipwa kinyume cha sheria

Nyongeza ya mshahara aliyopata Dkt. Mutua kwenye muhula wake wa pili KFCB ilibainika kuwa kinyume cha sheria.

Marion Bosire
2 Min Read
Ezekiel Mutua, Mkurugenzi Mtendaji MCSK

Aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Kuainisha Filamu nchini Kenya – KFCB, Dkt. Ezekiel Mutua ameagizwa arejeshe shilingi milioni 27 alizopokea kama mshahara katika muhula wake wa pili afisini.

Baraza la Rufaa la Mashirika ya Umma – SCAT lilidumisha uamuzi wa kaguzi ya mashirika ya umma – ISC wa kumtoza Dkt. Mutua pesa hizo baada ya kubainika kwamba nyongeza yake ya mshahara kutoka shilingi 348,840 hadi shilingi 1,115,850, ilikuwa kinyume cha sheria.

ISC ilisema kwamba mkataba mpya wa kazi wa Dkt. Mutua wa mwaka 2018 haukuwa sawa kwani haukuwa na mchango wa tume ya kuratibu mishahara na marupurupu nchini – SRC, Baraza la Ushauri la Mashirika ya Serikali – SCAC na Waziri.

Waziri wa wakati huo alikuwa amekataa mkataba huo mpya pamoja na pendekezo la kuongeza mshahara wa Dkt. Mutua lakini bodi ya KFCB ilitekeleza masharti hayo mapya ya mkataba.

Dkt. Mutua alijitetea akisema aliamini kwamba kuteuliwa kwake kuhudumu kwa muhula mwingine na kupata nyongeza ya mshahara vilikuwa sawa kisheria, kwa sababu havikupingwa na mamlaka husika wakati akihudumu katika KFCB.

Hata hivyo, Baraza la Rufaa la Mashirika ya Umma lilipata kwamba hatua zilizochukuliwa na bodi ya KFCB kama vile kupuuza michakato faafu ya kisheria, zilifanya mshahara huo kuwa kinyume cha sheria.

Mwanachama mmoja wa bodi ya KFCB kwa jina Nehemiah Kipkoech naye alitozwa fedha kwa jukumu alilotekeleza katika kuidhinisha nyongeza hiyo ya mshahara wa Mutua.

Baraza hilo lilihitimisha kwamba hatua ya bodi ya KFCB kukosa kufuata taratibu zinazofaa ilisababisha kupotea kwa fedha za umma, na hivyo kufuta nyongeza hiyo ya mshahara.

Share This Article