Rais wa zamani wa Malawi Peter Mutharika wa chama cha Democratic Progressive (DPP), angali anaongoza kwenye matokeo ya kura za urais wa nchi hiyo, akikaribia kumbwaga Rais wa sasa Dkt. Lazarus Chakwera wa chama cha Malawi Congress (MCP).
Kulingana na matokeo ya hivi punde, Mutharika, aliye na umri wa miaka 85, anakaribia kurejea mamlakani baada ya kushindwa na Chakwera katika uchaguzi uliopita.
Matokeo ya urais katika uchaguzi huo wa Jumatatu iliyopita yanatarajiwa kutangazwa kufikia mwishoni mwa juma hili.
Matokeo ya ujumuishaji kura unaofanywa na tume ya uchaguzi nchini Malawi yanaashiria Mutharika ametwaa ushindi katika maeneo mengi nchini humo dhidi ya Chakwera.
Hata hivyo, huenda raundi ya pili ya uchaguzi ikaandaliwa ili kubaini Rais mpya ikiwa kiwango kinachohitajika cha kura hakitafikiwa na mshindi wa uchaguzi huo.
Ili kutangazwa mshindi wa urais, mgombea lazima apate zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa.