Licha ya kuwa waandalizi wenza wa michuano ya CHAN ya mwaka huu, Marais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda hawakuwa uwanjani wakati timu zao zilipocheza mechi za ufunguzi za makundi yao.
Samia aliwashangaza wengi kwa kukosa kuhudhuria sherehe za ufunguzi Jumamosi iliyopita katika uwanja wa Benjamin Mkapa, na pia mechi ya ufunguzi ambapo Tanzania waliishinda Burkina Faso mabao 2-0 katika mechi ya kundi B.
Rais Samia, hata hivyo, aliwanunulia mashabiki jumla ya tiketi 10,000 kushuhudia mchuano huo wa Tanzania dhidi ya Burkina Faso.
Hatua hiyo imeibua maswali mengi kuliko majibu, ni kwa nini Marais Samia na Museveni walikosa kufika uwanjani bila kutoa sababu maalum.
Kwa kawaida, viongozi hao walitarajiwa kushuhudia mechi za ufunguzi katika nchi zao.
Museveni pia alikosekana uwanjani Mandela wakati Uganda Cranes waliposhindwa mabao 3-0 na Algeria katika mechi ya kwanza ya kundi C Jumanne.
Hata hivyo, Museveni aliwakilishwa na mkewe,Janet Museveni katika mechi hiyo ya ufunguzi.
Ni Rais William Ruto pekee kati ya viongozi wa mataifa matatu yanayoandaa dimba hilo aliyekuwa uwanjani Kasarani, wakati Kenya ikiwazidi maarifa DR Congo Jumapili iliyopita kwa bao 1-0 katika kundi A.