Rais Yoweri Museveni alitoa habari zilizowashangaza wengi kuhusu baba mzazi wa kweli wa mwanamuziki wa Uganda ambaye pia ni rais wa Shirikisho la kitaifa la Wanamuziki wa Uganda – UNMF, Edirisa Musuuza, maarufu kama Eddy Kenzo.
Awali mwanamuziki huyo alikuwa amemtaja babake mzazi kuwa Hassan Ssenyange ambaye alifariki mwaka 2012.
Museveni hata hivyo alifichua kwamba babake Kenzo wa kweli ni marehemu Chefe Ali, kamanda wa ngazi ya juu katika Jeshi la Ukombozi wa Kitaifa – NRA na baadaye Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda -UPDF.
Kabla ya kifo chake mwaka 1999, Chefe Ali, ambaye jina lake halisi ni Eriya Mwine, aliwahi kuhudumu kama Mkuu wa Majeshi wa UPDF na kamanda wa majeshi katika vikosi vitatu tofauti.
Wakati wa vita vya msituni, anakumbukwa zaidi kwa kuongoza Kikosi cha 11 ambacho kilizingira kambi ya Simba Battalion huko Mbarara mwaka 1985.
Museveni alitoa ufunuo huo wa kushangaza wakati wa uzinduzi wa Albamu ya Yoweri, mkusanyiko wa nyimbo uliotayarishwa na wanachama wa UNMF walioshirikisha watayarishaji na waandishi wa nyimbo kutoka kote nchini.
“Kenzo ni mtoto wa askari. Aliniambia yeye ni mtoto wa Chefe Ali,” Museveni alifichua.
Rais aliendelea kumuuliza Kenzo iwapo alikuwa ameweka wazi taarifa hiyo au la huku akimwomba atambulishe watoto wengine wa marehemu Chefe Ali na akaelezea jinsi wote wanavyofanana naye.