Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, amesema kuwa watu 42 walifariki kwenye maandamano ya Juni 25 na Julai 7, 2025 mtawalia.
Akiwahutubia wanahabari Jumatatu jioni Jijini Nairobi, Murkomen alisema takriban watu 600 walijeruhiwa, wakiwemo maafisa wa polisi 496 huku watu 1,500 wakikamatwa kwa kuhusika katika visa vya uhalifu vikiwemo ugaidi, mauaji, wizi wa kimabavu, dhuluma za kijinsia, uteketezaji na mashambulizi dhidi ya miundombinu.
“Wahalifu walilenga baadhi ya vifaa vya serikali, ikiwa ni pamoja na vituo vya polisi, magari ya serikali, afisi na hospitali,”alidokeza waziri huyo.
Aidha waziri huyo alisema serikali itabuni sera zitakazotoa mwongozo kwa maafisa wa usalama kuhusu utumizi wa nguvu na silaha wakati wa maandamano.
“Mipango inaendelea ya kutoa miongozo kwa maafisa wa polisi wanapokabiliana na waandamanaji,”alisema Murkomen.
Alikanusha kuwepo kwa kikosi maalum kinachowahangaisha wananchi, huku akiwaonya maafisa wa polisi dhidi ya kukiuka sheria wakati wa kukabiliana na waandamanaji.
Waziri huyo aliongeza kuwa afisa mmoja wa polisi anakabiliwa na mashtaka ya mauaji.