Murkomen: Vituo vyote vya Polisi vitawekwa kamera za CCTV

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen.

Wizara ya Usalama wa Taifa imekariri kujitolea kwake kufanikisha mpango wa marekebisho na kuimarisha uwajibikaji katika Huduma ya Taifa ya polisi.

Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, alitangaza kuwa katika muda wa miaka miwili ijayo, kamera za CCTV zitakuwa za lazima katika vituo vyote vya polisi kote nchini.

Katika hotuba yake kuhusu Usalama wa Taifa, Murkomen alisema hatua ya kuweka kamera hizo iliafikiwa baada ya mashauriano ya kina na pia kutokana na matukio ya awali na yale yanayoshuhudiwa sasa hasaa kuhusu utovu wa maadili miongoni mwa baadhi ya maafisa wa polisi.

“Sasa itakuwa ni lazima kwa vituo vyote vya polisi kuwa na Kamera za CCTV, kuimarisha uwazi na uwajibikaji.,” alisema Murkomen.

Tangazo hilo la waziri Murkomen linajiri kufuatia wasiwasi ulioibuliwa na umma kufuatia kifo cha Albert Ojwang mikononi mwa maafisa wa polisi.

Wakati huo huo, Murkomen alisema atapendekeza sheria itakayoharamisha hatua zozozte za kuvuruga kamera za CCTV kwenye vituo vya polisi.

Kulingana na Murkomen, maafisa wanaosimamia vituo vya polisi (OCS), ndio watahakikisha vifaa hivyo vinafanyakazi kikamilifu.

Share This Article