Murkomen: Visa vya wizi wa mifugo vimepungua kwa asilimia 70

Tom Mathinji
2 Min Read
Waziri wa usalama Kipchumba Murkomen, azindua magari ya polisi ya kivita katika makao makuu ya GSU mtaani Ruaraka.

Waziri wa usalama wa kitaifa Kipchumba Murkomen, amesema kuwa visa vya wizi wa mifugo na ujangili vimepungua kwa asilimia 70.

Kulingana na Murkomen, hatua hiyo imefanikishwa na kujitolea mhanga kwa maafisa wa polisi ambao hufanya kazi mazingira magumu.

Aliyasema hayo leo Alhamisi, alipozindua magari ya polisi ya vita katika Makao Makuu ya kitengo cha GSU mtaani Ruaraka.

Alikariri kujitolea kwa serikali kuendelea kuimarisha vifaa vya usalama, kuhakikisha usalama katika pembe zote za nchi.

“Magari haya ya kivita yatapiga jeki vita dhidi ya wizi wa mifugo na ujangili kaskazini mwa nchi na maeneo mengine nchini,” alisema Murkomen.

Maafisa wa polisi wapokea magari mapya kupiga jeki vita dhidi ya wizi wa mifugo na ujangili.

Kulingana na waziri huyo, mpango wa kuimarisha vifaa vya usalama unatokana na tishio la usalama linalosababishwa na mataifa jirani pamoja na visa vya wizi wa mifugo katika maeneo ya wafugaji humu nchini.

Aliwahakikishia maafisa wa polisi kuwa wizara yake itawasaidia wanapotekeleza majukumu yao, akisema wanaokiuka sheria na kanuni za Huduma ya Taifa ya Polisi (NPS), watachukuliwa hatua.

“Ninawahakikishia maafisa wa usalama kwamba wizara yangu itawasaidia mnapotekeleza majukumu yenu,” alidokeza waziri huyo.

Kuhusu mageuzi, Murkomen alibainisha kuwa yanalenga zaidi kuboresha mishahara, bima ya matibabu na maslahi ya afya ya akili ya maafisa hao.

Share This Article