Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, amethibitisha kujitolea kwa serikali kukabiliana na visa vya utovu wa usalama, akidokeza kuwa magenge ya wahalifu ni tisho kubwa kwa taifa hili.
Akizungumza katika kaunti ya Nakuru wakati wa ziara ya Jukwaa la Usalama, waziri huyo alidokeza kuwa visa vya utovu wa usalama huchochewa na utumizi wa mihadarati na ubugiaji mvinyo.
“Ikiwa tutakabiliana na mihadarati na unywaji wa pombe, basi tutapunguza athari za utovu wa usalama,” alisema Murkomen.
Aidha alielezea wasiwasi kuhusu kupungua kwa idadi ya wanafunzi wanaosajiliwa kwenye shule za kutwa, hasaa katika maeneo ambayo ni ngome ya magenge ya wahalifu.
“Ni jambo la kusikitisha kwamba baadhi ya shule zimeshuhudia upungufu wa idadi ya wanafunzi kutokana na kuwepo kwa makundi ya wahalifu,” alidokeza waziri huyo.
Murkomen, alielezea mipango ya kuimarisha kitengo cha Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kinachoshughulikia ulanguzi wa watu, hasaa watoto wanaotumiwa katika biashara ya ngono kama sehemu ya mpango mpana wa kuhakikisha udumishaji usalama na kuzingatia haki za kibinadamu.