Operesheni ya kitaifa almaarufu ‘Ondoa Jangili’, itaendelea katika juhudi za kudumisha utulivu katika maeneo ambayo yanakabiliwa na ukosefu wa usalama kote nchini, hayo ni kwa mujibu wa Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen.
Murkomen alisema wasiwasi kuhusu kuibuka kwa makundi ya majangili, utumizi wa dawa za kulevya na ulanguzi wa binadamu umetanda katika kaunti ya Isiolo.
Alipokuwa katika ziara ya kukagua hali ya usalama kwenye kaunti ya Isiolo leo Alhamisi, waziri huyo alidokeza kuwa kundi la maafisa wa usalama kutoka asasi mbali mbali, limeimarisha operesheni za kuvunja mitandao ya wahalifu katika eneo hilo kupitia mkakati wa ‘Ondoa Jangili’.
Aidha waziri huyo alisema operesheni hiyo imefanikisha kupatikana kwa bunduki 46 na bangi ya thamani ya shilingi milioni 10.
Wakati huo huo, Murkomen alisema washukiwa wanne waliokuwa na silaha walikamatwa, huku wengine tisa wakitiwa nguvuni wakishiriki ulanguzi wa bangi na binadamu kutoka nchi moja jirani.
Aliwaagiza Machifu na Manaibu wao kuifanyia serikali kazi na kukoma kufuata maagizo ya wanasiasa ambao wanamaslahi ya kibinafsi.
Murkomen alikuwa ameandamana na kamishna wa eneo la Mashariki Paul Rotich, maafisa wakuu wa serikali ya kitaifa na maafisa wakuu wa usalama wa eneo hilo.