Murkomen awapongeza polisi kwa kudumisha utulivu wakati wa maandamano

Tom Mathinji
2 Min Read
Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen na Katibu katika wizara hiyo Dr. Raymond Omollo, wazungumza na maafisa wa polisi siku ya maandamano ya Saba Saba Jijini Nairobi.

Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, amewapongeza maafisa wa usalama kwa jukumu walilotekeleza la kulinda mali na maisha wakati wa maandamano ya Saba Saba Jumatatu Julai 7,2025.

Aidha waziri huyo alilalamika kuwa maandamano hayo yaliingiliwa na wahalifu waliolenga kuzua ghasia, uharibifu na uporaji wa mali.

“Jambo la kusikitisha ni kwamba, maandamano ya amani yametekwa nyara na wahalifu ambao lengo lao ni kuzua ghasia na kusababisha uharibifu,”alisema waziri huyo.

Murkomen aliwapongeza maafisa wa usalama kwa juhudi zao za kupunguza visa vya ghasia, uporaji na uharibifu wa mali ya umma wakati wa maandamano hayo ya Jumatatu, ikilinganishwa na jinsi hali ilivyokuwa wakati wa maandamano ya Juni 25,2025.

“Tumejitolea kuhakikisha waandamanaji wanadumisha amani na nidhamu wakati wa maandamano,”alidokeza waziri Murkomen.

Wakati huo huo, Murkomen alithibitisha kuwa wale waliohusika na visa vya uhalifu wakati wa maandamano ya Juni 25,2025, tayari wamefunguliwa mashtaka mahakamani, huku akisema waliohusika na visa vya ghasia na uhalifu wakati wa maandamano ya Saba Saba, pia watachunguzwa na kufunguliwa mashtaka.

“Wahalifu waliosababisha ghasia wakati wa maandamano ya Juni 25, wameshtakiwa mahakamani. Wale pia waliohusika na maandamano ya leo (Saba Saba), pia watachunguzwa na kushtakiwa,” alidokeza waziri huyo.

Kulingana na Huduma ya Taifa ya Polisi, watu 11 walifariki, maafisa wa polisi 52 na raia 11 walijeruhiwa huku watu 567 wakimatwa kwenye maandamano ya Saba Saba siku ya Jumatatu.

Share This Article