Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, ametoa onyo kali kwa wanasiasa na maafisa wa serikali wanaofanikisha ulanguzi wa mihadarati hapa nchini, akisema watachukuliwa hatua za kisheria.
“Wanasiasa hawatakubaliwa kuwatisha maafisa wa serikali au Maafisa wa Polisi, Machifu na Manaibu wao wakati washukiwa wanapokamatwa. Maafisa watakaojihusisha na uovu huo hawatasazwa,” alisema waziri Murkomen alipokuwa akikamilisha ziara yake ya Jukwaa la Usalama katika kaunti ya Embu.
Waziri huyo alielezea wasiwasi kuhusu utumizi wa dawa na pombe zilizoharamishwa akisema kuwa operesheni imeanzishwa dhidi ya wanaojihusisha na biashara hiyo haramu.
Alidokeza kuwa eneo la Mlima Kenya limeghubikwa na utumizi wa mihadarati katika kaunti za Meru, Tharaka Nithi na Embu.
“Pombe haramu na ulanguzi wa mihadarati ni maarufu sana katika eneo hili. Tumeshirikiana na Shirika la Huduma za Wanyamapori Nchini kukabiliana na wale wanaokuza bangi msituni,” alisema waziri huyo.