Murkomen atoa tamko ukarabati wa Uwanja wa Kasarani

Francis Ngala
2 Min Read

Waziri wa Michezo Kipchumba Murkomen ana matumaini kwamba ukarabati unaoendelea kufanywa katika uwanja wa Kimataifa wa Michezo wa Moi Kasarani, utakamilika kwa wakati mzuri kama ilivyopangwa kabla ya Michuano ya Mataifa ya Afrika (CHAN) mwaka ujao.

Murkomen ambaye alizungumza baada ya ziara ya ukaguzi ya uwanja huo wa kimataifa alisema wafanyikazi kwenye eneo hilo wanafanya kazi usiku na mchana ili kumaliza ukarabati huo kwa wakati ufaao.

“Niko na imani kuwa, mkandarasi akitekeleza ratiba ya kufanya kazi kwa saa 24, uboreshaji wa uwanja huo utakamilika ndani ya muda uliowekwa,” alisema Murkomen.

Miongoni mwa kazi zinazoendelea kufanywa katika uwanja huo wenye uwezo wa kubeba mashabiki 60,000, ni pamoja na ufungaji wa dari mpya na mfumo wa taa, Nyasi pia zinaendelea kupandwa ardhini.

Uwanja wa Michezo wa Moi Kasarani

Kenya, Uganda na Tanzania watakuwa wenyeji wa michuano ya CHAN kuanzia Februari mosi 1-28, mwaka 2025.

Ziara ya waziri Murkomen ina ujio, huku kukiwa na ukaguzi uliopangwa na maafisa wa CAF ambao wako nchini kwa sasa.

Maafisa wa CAF humu nchini wanaongozwa na Mkuu wa Kitengo cha Usalama cha CAF Christian Emeruwa ambao wamezuru chini kwa ajili ya zoezi la pili la ukaguzi.

Miongoni mwa vitu muhimu wanavyotathmini ni pia hoteli kubwa kubwa zilizo jijini Nairobi ambazo zimepangwa kutosheleza timu na maafisa watakaokuja na timu zao kwa michuano hiyo.

Walikagua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) siku ya Jumanne.

Kando na Kasarani, uwanja wa Nyayo wenye uwezo wa kubeba mashabiki 18,000 pia unafanyiwa marekebisho.

Uwanja mpya pia wa Talanta ulio eneo la Jamhuri, Hapa Nairobi na ulio na uwezo wa kubeba mashabiki 55,000 unaendelea na utakamilika ifikapo Disemba mwakani , 2025.

Share This Article
Follow:
I am Versatile Multimedia Journalist with years of experience in Digital platforms, Live TV and Radio. In another world am a News Anchor and Reporter.