Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, ametangaza kubuniwa kwa jopo litakalomteua Mwenyekiti na Makamishna saba wa Tume ya Mshikamano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC).
Kulingana na Murkomen, muda wa kuhudumu wa maafisa wa sasa wa Tume hiyo inayoongozwa na Rev. Samuel Kobia, utakamilika Novemba 17, 2025, na kuhitimisha muhula wa miaka sita ulioanza Novemba 2019.
“Kuna nafasi wazi katika uanachama wa tume hiyo kutokana na kukamilika kwa muda wa kuhudumu wa miaka sita wa wanachama wa sasa,” alisema Murkomen kupitia gazeti rasmi la serikali toleo la Novemba 4, 2025.
Jopo hilo la wanachama saba, litajukumiwa kuwatafuta wanaofaa kuchukua hatamu za uongozi kwenye tume hiyo.
Wanachama wa jopo hilo ni pamoja na Reuben Chirchir, Francis Meja, Pauline Mcharo, Col. (Rtd.) Alfred Mshimba, Michael Nzomo Mbithuka, na Rtd. Lady Justice Hannah Okwengu.
Tume ya NCIC imejukumiwa kuhakikisha mshikamano wa kitaifa, fursa sawa utangamano wa amani miongoni mwa wakenya wa tabaka mbali mbali na kidini.