Serikali imefanikiwa kuokoa Wakenya 18 waliokuwa katika hali hatari baada ya kujiunga na vikosi vya Russia katika vita na Ukraine.
Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, alisema Wakenya hao 18 wamepewa hati za dharura za kusafiri kurejea nchini.
Mudavadi ambaye pia ni waziri wa Mambo ya Nje, alisema zaidi ya Wakenya 200 wanaaminika kuajiriwa na makundi yanayodaiwa kufanya kazi nchini Kenya na Russia.
Alidokeza kuwa Ubalozi wa Kenya mjini Moscow umethibitisha kuwa baadhi ya Wakenya hao wamejeruhiwa katika vita, huku wengine wakibaki bila msaada baada ya kujaribu kuajiriwa.
Serikali inashirikiana na serikali ya Russia kuhakikisha Wakenya wote, wakiwemo wale walioko kwenye kambi za kijeshi, wanapelekwa salama kwenye ubalozi wa Kenya mjini Moscow kisha kurejeshwa nyumbani.
Aidha, serikali inashirikiana na serikali ya Ukraine kuhakikisha Wakenya waliokuwa wafungwa wa kivita wanachukuliwa salama na kurejeshwa nchini.
Mudavadi aliwaonya Wakenya wote wanaotafuta kazi za kigeni kuhakiki uhalali wa wanaotoa nafasi za ajira kabla ya kukubali ajira yoyote.