Waziri mwenye Mamlaka Makuu aliye pia Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi, amesema serikali ya Kenya ni dhabiti na imejitolea kutimiza ahadi zake kwa wananchi bila kubabaishwa na kelele za kisiasa zilizopo.
Akizungumza na raia wa Kenya wanaoishi katika miji ya Rabat, Casablanca, Marrakech na Kenitra nchini Morocco, Mudavadi aliwahakikishia kuwa licha ya misukosuko ya kisiasa nchini Kenya, serikali inaendelea kutekeleza miradi yake ya maendeleo.
“Msibabaishwe na yale mnayoyashuhudia Kupitia mitandao ya kijamii kuhusu yanayojiri nyumbani, ni kelele tu za baadhi ya watu. Serikali ambayo Iko mamlakani kwa muda wa miaka miwili sasa, inajizatiti kutekeleza majukumu yake kwa mamilioni ya wakenya,” alisema Mudavadi.
Aidha Mudavadi alielezea hatua zilizopigwa na serikali kama vile ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, na mpango wa Afya kwa wote UHC ambao umewasajili zaidi ya wakenya million 21 kwa Hazina ya Afya ya Jamii SHIF, hii ikiwa ni ongezeko ikilinganishwa na idadi ya milioni 9 iliyokuwa hapo awali kwa Hazina ya NHIF.
Hata hivyo alikiri kuwepo kwa baadhi ya changamoto katika utekelezaji wa miradi ya serikali, akielezea matumaini kuwa miradi hiyo itakamilika.
Aliwahikiza wakenya wanaoishi ughaibuni kuwa mabalozi wema wa taifa hili katika nchi wanakoishi, wanapoendelea na masomo, kazi na hata biashara.