Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi amewahakikishia washirika wa kidiplomasia na wawekezaji kuwa Kenya ni taifa lililojikita kwenye miongozi thabiti ya katiba.
Alisema serikali ya Kenya huzingatia sheria zilizopo katika kukuza uongozi wa kidemokrasia na umoja wa kitaifa.
Mudavadi alisema Kenya imeendelea kunufaika kutokana na ushirikiano kati yake na mataifa mengine kufanikisha maendeleo endelevu.
“Tumejitolea kama serikali kuhakikisha mazingira thabiti ya uwekezaji na ushirikiano,”alisema Mudavadi.
Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, alidokeza kuwa katiba ya Kenya ya mwaka 2010 inawalinda watu wote, familia, jamii na taifa nzima kwa jumla, na serikali kamwe haitakiuka mapenzi ya wananchi.
Akitaja Kenya kuwa nchi yenye demokrasia thabiti, Mudavadi alisisitiza kuwa Kenya huandaa uchguzi mkuu kila baada ya miaka tano kwa kuzingatia sheria kikamilifu, akitaja kubuniwa upya kwa Tume ya Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kama uthibitisho katika kulinda uongozi wa kidemkrasia na maadili ya kitaassi.
Mudavadi aliyasema hayo alipoongoza sherehe za 145 za siku ya kitaifa ya Kifaransa baada ya kualikwa na balozi wa Ufaransa hapa nchini Arnaud Suquet katika ubalozi wa nchi hiyo jijini Nairobi.