Huku uchaguzi wa wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) ukitarajiwa kufanywa mwishoni mwa wiki hii, Waziri Mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi tayari amewasili jijini Addis Ababa nchini Ethiopia kumpigia debe mwaniaji wa Kenya kwenye wadhifa huo Raila Odinga.
“Tukiwa katika mkondo wa mwisho, nitajihusisha katika kampeni za kutafuta uungwaji mkono wa Raila kutoka kwa Marais. Uongozi wa Raila katika wadhifa huo, utainua hadhi ya Kenya na kuimarisha sauti ya bara Afrika katika jukwaa la ulimwengu,” alisema Mudavadi.
Raila anakabiliana na wawaniaji wengine wawili ambao ni Richard Randriamandrato wa Madagascar na Mahamoud Ali Youssouf wa Djibouti katika uchaguzi huo.
Wawaniaji hao watatu wanalenga kumrithi mwenyekiti anayeondoka Moussa Faki Mahamat ambaye amehudumu kwa mihula miwili.
Katika kampeni zake za kuwania wadhifa huo, Raila alisema lengo lake kuu ni kuboresha miundombinu, uchumi, biashara baina ya nchi za Afrika na usawa wa kijinsia barani humu.
Mudavadi pia atahudhuria mkutano wa 46 wa Baraza Kuu la Umoja wa Afrika (AU), ambapo Mawaziri wa Mambo ya Nje watawachagua makamishna wa AUC.