Mudavadi asisitiza uhusiano kati ya Kenya na Marekani ni thabiti

Marion Bosire
2 Min Read
Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi.

Waziri aliye na mamlaka makuu ambaye pia ni waziri wa masuala ya nchi za kigeni Musalia Mudavadi amesisitiza kwamba uhusiano mwema unaendelea kati ya Marekani, baada ya taifa hilo lililostawi kujiondoa kwenye kongamano la G20.

Kulingana na Mudavadi, Kenya imejitolea kuendeleza uhusiano thabiti na wa kudumu na Marekani, hata wakati dunia ikishuhudia vichwa vya habari kuhusu uamuzi wa Rais Donald Trump kuzuia maafisa wa Marekani kuhudhuria mkutano ujao wa G20 jijini Johannesburg, nchini Afrika Kusini.

Agizo hilo, ambalo limesababisha kufutwa kwa ziara iliyopangwa ya Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance nchini Kenya mwisho wa mwezi huu, limevutia umakini wa kimataifa.

Hata hivyo, Kenya imesalia thabiti, ikisisitiza kuwa ushirikiano na Marekani utaendelea kupitia njia zilizowekwa za kidiplomasia.

Makamu wa Rais Vance alikuwa amepangiwa kuongoza ujumbe wa Marekani katika kongamano la G20 kabla ya kuelekea Nairobi kwa mazungumzo ya ngazi ya juu kuhusu biashara, usalama na uwekezaji.

Ingawa ziara hiyo haitafanyika mwezi huu, maafisa wa Kenya wanasema ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili bado uko imara.

Mudavadi alisema, “Kenya na Marekani zinafurahia uhusiano wa kina na wa kihistoria uliojengwa juu ya kuheshimiana, maadili ya kidemokrasia yanayoshirikishwa na maslahi ya pamoja.”

Aliongeza kusema kwamba hata ingawa mabadiliko ya ratiba hutokea mara kwa mara katika diplomasia, ushirikiano wa Kenya na Marekani unaendelea kuwa thabiti katika sekta zote.

Share This Article