Waziri aliye na mamlaka makuu Musalia Mudavadi ameutaka uongozi mpya wa Umoja wa Afrika ushughulikie changamoto mbali mbali zinazokabili bara hili.
Akizungumza na wanahabari jijini Addis Ababa nchini Ethiopia jana, Mudavadi alisema hatua za haraka zinahiajika katika kushughulikia changamoto za amani na usalama.
Mudavadi alitaja mataifa ya DRC, Sudan, Sudan Kusini na eneo la Sahel kama maeneo yanayokumbwa na changamoto za amani na usalama.
Kulingana naye, nchi nyingine za ulimwengu zinashughulikia changamoto nyingine na hivyo ni muhimu Afrika iwe mstari wa mbele kutafuta suluhu zake.
Waziri Mudavadi alisema pia kwamba Umoja wa Afrika unafaa kuharakisha na kutathmini jinsi hali tete ya siasa za kijiografia inaweza kuathiri sekta za viwanda na kilimo barani Afrika.
Mudavadi alisema pia kwamba Umoja wa Afrika unafaa kuwaza kuhusu kuunga mkono mipango inayotekelezwa na China barani humu, akitaja nchi hiyo kuwa mshirika muhimu wa kuhakikisha ufanisi wa eneo biashara huria barani Afrika.
Matamshi ya Mudavadi yanajiri muda mfupi baada ya kongamano kuu la Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa nchini Ethiopia ambapo pia uchaguzi wa viongozi wapya uliandaliwa.
Kenya ilikuwa imewasilisha mgombea wa wadhifa wa mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika AUC Raila Odinga ambaye alishindwa na Mohamud Ali Youssouf wa Djibouti.