Muda wa agizo la kuzuia CAK kuzuia matangazo mubashara ya maandamano waongezwa

Jaji wa mahakama kuu Chacha Mwita aliongeza muda huo hadi Oktoba 27, 2025.

Marion Bosire
2 Min Read

Mahakama kuu ya Kenya imeongeza muda wa agizo ambalo ilitoa awali la kuzuia mamlaka ya mawasiliano nchini CAK kuzuia vyombo vya habari kupeperusha matangazo ya moja kwa moja ya maandamano.

Katika kikao cha kutaja kesi hiyo jana Jumatano Julai 2, 2025, Jaji Chacha Mwita alielekeza kwamba kesi hiyo itajwe tena tarehe 27 mwezi Oktoba mwaka huu wa 2025.

Kulingana na mahakama, kuongezwa kwa muda wa agizo hilo kunalenga kutoa fursa kwa kesi iliyowasilishwa na chama cha mawakili nchini LSK, chama cha wahariri wa habari nchini KEG na Katiba Institute isikilizwe na kuamuliwa.

Jumatano Juni 25, 2025 makundi hayo matatu yalikwenda mahakamani kupinga agizo la CAK la kukomesha matangazo ya moja kwa moja ya maandamano na hatua ya kuzima mawimbi ya baadhi ya vyombo vya habari.

Hata hivyo mamlaka ya mawasiliano ilielezea mahakama jana kwamba agizo hilo la Juni 25, 2025 halikuwa la kudumu, kulingana na mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya mawasiliano, lililenga kutuliza hali ya wasiwasi.

Akizungumza mbele ya jaji Chacha Mwita, mkurugenzi mkuu wa CAK David Mugonyi alitetea hatua waliyochukua akisema inakubalika ulimwenguni kote kama njia ya kupunguza madhara ya wasiwasi unaotokana na matangazo ya moja kwa moja.

Jaji aliagiza wahusika wa kesi hiyo kuweka pamoja maombi yao kwa mahakama na kusubiri maelekezo zaidi Oktoba 27, 2025.

Share This Article