Mtoto Pendo: Mahakama yatoa amri ya kukamatwa kwa afisa wa polisi

Tom Mathinji
2 Min Read
Idara ya Mahakama

Mahakama Kuu imetoa agizo la kukamatwa kwa afisa wa cheo cha juu wa polisi, Mohammed Baa, aliyehusishwa na kifo cha mtoto Pendo mwaka 2017.

Agizo hilo limetolewa leo Alhamisi, baada ya Baa kukosa kufika mahakamani. Alitarajiwa kufunguliwa mashtaka pamoja na wenzake, kwa mauaji ya mtoto Pendo katika kijiji cha Nyalenda kaunti ya Kisumu wakati wa machafuko ya baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2017.

Baa alifunguliwa mashtaka pamoja na wengine 11 ambao ni; Titus Yoma, Titus Mutune, John Chengo, Linah Kogey, Benjamin Koima, Benjamin Lorema, Volker Edambo, Cyprine Robe, Josphat Sensira, Mohammed Ali Guyo na James Rono.

Lady Justice Lilian Mutende, alimwagiza Inspekta Jenerali wa polisi  Douglas Kanja kutekeleza agizo hilo na kumwasilisha Baa mahakamani, ili ajibu mashtaka.

Baa, na wenzake 11, mara kadhaa wamekosa kufika mahakamani, licha ya maagizo ya kukamatwa kwao kutolewa.

Wakati wa kutajwa kwa kesi hiyo Alhamisi, naibu msaidizi mkuu wa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Vincent Monda, aliwasilisha mahakamani maagizo ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Renson Ingonga, yaliyowataka washatakiwa hao wote kuwa mbele ya mahakama kabla ya kujibu mashtaka, na sio haki kwa Baa kutofika mahakamani.

“Mkurugenzi wa mashtaka ya umma ametuagiza kufahamisha mahakama kwamba washukiwa hao wote lazima wawe mahakamani kujibu mashtaka,” alisema Monda.

Mahakama hiyo imetenga Novemba 5, 2024 kuwa siku ya washukiwa hao kujibu mashtaka, na kwamba Baa anapaswa kuwasilishwa mahakamani siku hiyo kuambatana na agizo la kukamatwa kwake.

TAGGED:
Share This Article