Wanafunzi wa kidato cha nne nchini wameanza rasmi mtihani wa kitaifa (KCSE) wa mwaka 2025, baada ya majaribio ya siku ya Ijumaa iliyopita.
Leo Jumanne, watahiniwa hao wanafanya mitihani ya mahojiano ya masomo ya Kifaransa, Kijerumani, Kiarabu, Lugha ya ishara ya Kenya na vitendo vya somo la muziki.
Mitihani ya masomo ya kuandikwa itaanza Novemba 4 na kukamilika Novemba 21, baada ya kukamilika kwa mitihani ya mahojiano na ya vitendo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Kenya (KNEC), David Njengere, amesema kuwa zaidi ya watahiniwa 996,000 watafanya mtihani huo.
Njengere alitoa hakikisho kuwa maandalizi ya kina yamefanyika ili kuhakikisha mtihani huo unaendelea kwa utulivu na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wale watakaopatikana wakijihusisha na udanganyifu wa mitihani.
Wakati huo huo, wanafunzi 1,298,089 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kitaifa wa Gredi ya sita, KPSEA wiki ijayo, huku 1,130,669 wakitarajiwa kufanya mtihani wa kitaifa wa Gredi ya tisa (KJSEA).