Mtangazaji wa redio Edward Carey Kwach, ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 50.
Kulingana na taarifa kutoka Kwa msemaji wa familia Michael Okwiri, Kwach alifariki usiku wa April 28, 2025, alipokuwa akitibiwa ugonjwa meningitis.
“Ni kwa huzuni kubwa tunatangaza kifo cha ndugu yetu Carey,” ilisema taarifa hiyo ya familia.
Kwach, ambaye sauti yake ilitamba kwenye mawimbi ya taifa hili, atakumbukwa sana kwa miziki ya ubora wa hali ya juu aliyocheza, ambayo iliwavutia wasikilizaji kutoka pembe zote za taifa hili.
“Atakumbukwa kwa ucheshi na pia Kwa kuchagua miziki iliyoleta furaha na kuwafariji wengi,” iliongeza taarifa hiyo.
Wafanyakazi wenza na marafiki walimwomboleza Kwach mwenye mitandao ya kijamii.
Kifo chake kinajiri siku chache baada ya familia yake kuitisha usaidizi wa damu, alipokuwa amelazwa hospitalini.
Miongoni mwa vituo vya redio ambavyo amefanyia kazi ni pamoja na Hot 96 FM, Nation FM, Capital FM, Homeboyz Radio na hadi kifo chake alikuwa mfanyakazi wa Spice FM.