Mtangazaji nguli Omuga Kabisae afariki

Kabisae aliaga dunia Jumatatu usiku baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Marion Bosire
1 Min Read

Familia ya aliyekuwa mtangazaji mahiri wa KBC Radio Taifa Charles Omuga Kabisae imetangaza kifo chake kilichotokea usiku wa Jumatatu, tarehe 11 mwezi huu wa Agosti mwaka 2025.

Kabisae aliaga dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Omuga alianza safari yake ya utangazaji mwanzo wa miaka ya 1980 wakati huo akianzia katika kituo cha redio cha muda kilichokuwa kikipeperusha matangazo yake kwa lugha ya mama.

Alitiwa motisha kujiunga na taaluma ya utangazaji akiwa na umri mdogo baada ya kusikiliza watangazaji wa awali kama Leonard Mambo Mbotela, Job Isaac Mwamto, Hassan Madzoa, Stephen Desanjo na wengine.

Katika mahojiano yapata miaka mitano iliyopita, Omuga alisimulia kuhusu kisa cha kushangaza kilichomtokea kazini wakati akitekeleza kazi aliyofahamika kwayo zaidi ambayo ni matangazo maalumu na matangazo ya vifo.

Alisema walipokea tangazo la kifo ambalo alilishughulikia ipasavyo lakini dakika chache baadaye, waliokuwa wamewasilisha tangazo hilo wakarejea na kumtaka asahihishe wakidai kwamba jamaa yao alifufuka.

Omuga alielezea kwamba alirejelea tangazo la kufufuka kwa jamaa huyo mara kadhaa hewani kisa kilichomshangaza sana.

Kando na matangazo ya vifo, Omuga aliwahi kuendesha vipindi mbalimbali vya burudani katika KBC Radio Taifa ambayo awali ilifahamika kama Idhaa ya Taifa.

Wengi watamkosa kwa weledi wake katika utangazaji wa lugha ya Kiswahili.

Share This Article