Jamii ya watangazaji na wanahabari nchini na hasa wale wa shirika la utangazaji nchini KBC, inaomboleza kifo cha ghafla cha mwanahabari na mtangazaji Festus Amimo.
Kabla ya mauko, Amimo alikuwa akihudumu kama mkuu wa kituo cha redio cha Mayienga kinachomilikiwa na KBC na ambacho hurusha matangazo yake kwa lugha ya dholuo.
Taarifa za ndani kuhusu jinsi mauko yalimfika mapema leo bado hazijatolewa lakini mkurugenzi mkuu wa KBC Agnes Kalekye, anashirikiana na familia kufahamu mengi kuhusu matukio ya nyakati za mwisho mwisho za Festus.
Amimo wa miaka 46, alijiunga na KBC mwaka 2004 ambapo alianzia kazi katika tawi la Kisumu kabla ya kuhamia Nairobi punde baada ya Mayienga Fm kuanzishwa.
Kifo chake kimeshtua wengi katika tasnia ya uanahabari huku wanahabari wenza, wasikilizaji wa redio na hata viongozi wakitoa jumbe zao za rambi rambi.
Bi. Kalekye alimsifia mwendazake akimtaja kuwa mtangazaji aliyejitolea kwa kazi yake ambapo alikuwa akiendesha kipindi cha alfajiri kati ya saa 11 na saa 4 asubuhi.
Mkuu wa kitengo cha redio katika shirika la KBC Mary Daraja, alimkumbuka Amimo kama mtangazaji bora na aliyejitolea kwa dhati kwa kazi yake na ambaye uongozi wake wa kipekee uliinua kituo cha redio cha Mayienga.
Katibu wa usalama wa ndani Raymond Omollo ni mmoja wa viongozi wa serikali waliotoa jumbe za rambi rambi kufuatia kifo hicho cha ghafla cha Amino.
Omollo alimtaja Amimo kuwa mtu mzuri na rafiki wa kweli ambaye ukarimu wake na unyenyekevu viligusa kila mmoja aliyekuwa karibu naye.