Maafisa wa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori hapa nchini (KWS), kwa ushirikiano na Shirika la Msalaba Mwekundu, wamemwokoa mtalii wa hapa nchini aliyeanguka kwenye sehemu ya chini katika Mbuga ya Kitaifa ya Mlima Longonot.
Kupitia ukurasa wa X, KWS imesema mtalii huyo Bildad Simiyu alianguka pembeni mwa mwamba na hivyo ilikuwa vigumu kwa waokoaji kumfikia.
“Giza lilipoingia ilikuwa hatari kuendelea na shughuli ya uokoaji, lakini maafisa wetu wa KWS walikita kambi katika eneo hilo wakiendelea kumjulia hali mwathiriwa, wakimhakikishia kuwa mambo yatakuwa shwari,” lilisema shirika hilo.
Baada kupambazuka, waokoaji wa KWS walisaidiwa na maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu, Kikosi cha wazima moto cha Nakuru na maafisa wa polisi.
Mwendo wa saa tisa alasiri, Simiyu aliokolewa na alikuwa amejeruhiwa mguu wake wa kushoto.
Kwa sasa anapokea matibabu katika hospitali ya Naivasha.