Mswada wa adhabu ya kifo unaolenga wahusika wa ugaidi ulipitishwa mara ya kwanza katika bunge la Israel.
Wadadisi wanahisi kwamba adhabu ya kifo itatumiwa hasa dhidi ya Wapalestina wanaoua Wayahudi na sio wapiganaji wa Kiyahudi wanaoshambulia Wapalestina.
Waziri wa Usalama wa Taifa wa Israel, Itamar Ben-Gvir, amekuwa akitaka kwa muda mrefu mswada wa sheria unaoanzisha adhabu ya kifo kwa ‘magaidi’.
Marekebisho ya kanuni za adhabu, yaliyopendekezwa na Waziri wa Usalama wa Taifa wa mrengo wa kulia Itamar Ben-Gvir, yaliidhinishwa kwa kura 39 dhidi ya 16 katika Bunge lenye wabunge 120 Jumatatu.
Hiyo ni ishara kwamba marekebisho hayo yanapata uungwaji mkono kutoka kwa serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.
Kwa mujibu wa rasimu ya maandishi, adhabu ya kifo itatolewa kwa mtu yeyote anayemuua raia wa Israeli kwa sababu za kibaguzi na kwa lengo la kudhuru Israel na ufufuo wa wayahudi katika ardhi yao.
Wakosoaji walisema maneno hayo yanamaanisha kwamba kwa vitendo, adhabu ya kifo itawahusu karibu kabisa Wapalestina wanaoua Wayahudi, na si wapiganaji wa Kiyahudi wanaofanya mashambulizi dhidi ya Wapalestina.
Katika taarifa, shirika la Amnesty International lililaani hatua hiyo.
“Hakuna namna ya kupamba jambo hili; wabunge 39 wa Knesset waliidhinisha katika usomaji wa kwanza mswada unaoamuru mahakama kutekeleza adhabu ya kifo hasa dhidi ya Wapalestina” alisema Erika Guevara Rosas, mkurugenzi mkuu wa utafiti, utetezi, sera na kampeni wa shirika hilo.
Aliongeza kuwa adhabu ya kifo haifai kutolewa katika hali yoyote hata kutumiwa kama silaha ya ubaguzi na chombo cha serikali cha mauaji, utawala na ukandamizaji.
Afisa huyo mwandamizi wa Amnesty alielezea hatua ya bunge la Israel kuwa hatari na ya kurudisha nyuma sana na matokeo ya hali ya kutoadhibiwa kwa mfumo wa ubaguzi wa rangi wa Israel na mauaji ya halaiki huko Gaza.
Juhudi za kuanzisha sheria kama hiyo zimewahi kushindikana awali. Mswada wa sasa lazima upitishwe katika usomaji wa pili na wa tatu kabla haujawa sheria.
Taarifa kutoka Kamati ya Usalama wa Taifa, ambayo inajumuisha maelezo ya mswada huo, ilisema lengo lake ni kukomesha ugaidi kutoka kwenye mizizi na kuleta kizuizi kikubwa.