Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, ametoa wito kwa Wakenya kuheshimu uhuru unaoshuhudiwa hapa nchini.
“Tunaposema Kenya ni taifa lenye demokrasia, wengi huwa hawaamini. Nimetambua kwamba watu kutoka mataifa mengine huja hapa kuandamana na wanalindwa na katiba ya Kenya, hawadhulumiwi na yeyote,” alisema Mudavadi.
“Nchini Kenya, watu humtusi Rais, na katiba hulinda uhuru wao. Wengine hudai kwamba Kenya chini ya Rais Ruto inaongozwa kwa njia ya kiimla. Walijaribu kupeleka tabia yao katika nchi moja jirani na mlishuhudia kilichofanyika,” aliongeza waziri huyo wa Mambo ya Nje.
Mudavadi alitahadharisha kuwa, Wakenya wanapoingia katika nchi za kigeni, wanapaswa kutii sheria za mataifa hayo.
“Nimekuwa nikiwashauri vijana wa hapa nchini kwamba, wanapoabiri na kuingia nchi za kigeni, sheria za Kenya husitishwa na sheria za mataifa hayo huchukua usukani,” aliongeza Mudavadi.
Mudavadi aliyasema hayo alipohudhuria mazishi ya Mzee Mwalimu William Lumati, baba mzazi wa chansela mpya wa chuo kikuu cha Co-operative, Benard Chitunga, katika kaunti ndogo ya Malava, kaunti ya Kakamega.