Maafisa wa kukabiliana na ulanguzi wa mihadarati katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), wamemkamata mwanamake akijribu kusafirisha mihadarati kuelekea nchini India.
Mshukiwa huyo Caroline Wanjiku Mwangi mwenye umri wa miaka 25, alitiwa nguvuni alipokuwa akiabiri ndege iliyokuwa ikielekea Goa, nchini India.
Idara ya kukabiliana na makosa ya jinai DCI kupitia ukurasa wa X, ilisema maafisa wake walipofungua mkoba wa mwanamke huyo walipata kilo 1.3 za dawa za kulevya aina ya Cocaine.
“Baada ya kufungua mkoba wake maafisa wa DCI, walipata dawa hizo zikiwa zimepakiwa vyema. na baada ya kufanyiwa uchunguzi, matokeo yalibainisha kuwa zilikuwa ni dawa za kulevya aina ya Cocaine zenye uzani wa kilo 1.3,’ ilisema DCI.
Kwa sasa mshukiwa huyo anazuiliwa katika kituo cha polisi cha uwanja wa ndege wa JKIA, akisubiri kufikishwa mahakamani.
Dawa hizo pia zinazuiliwa na zitatumika kama ushahidi.