Mshukiwa wa mauaji Canada ashtakiwa

Jamaa huyo aliendesha gari lake kuelekea kwa umati wa watu jijini Vancouver nchini Canada ambapo aliua takribani watu 11.

Marion Bosire
2 Min Read

Mshukiwa ameshtakiwa kwa mauaji ya watu wanane baada ya gari kuogonga watu kadhaa waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya tamasha la barabarani la kusherehekea utamaduni wa Ufilipino, jijini Vancouver nchini Canada.

Jumamosi usiku, jamaa huyo aliendesha gari lake kuelekea kwa umati wa watu jijini Vancouver nchini Canada ambapo aliua takribani watu 11 katika kile ambacho polisi wamekitaja kuwa siku mbaya zaidi katika historia ya jiji hilo.

Baadhi ya waliokuwa wakihudhuria tamasha hilo walimkimbiza na kumkamata mshukiwa aliyetambuliwa kama Kai-Ji Adam Lo wa umri wa miaka 30, mkazi wa Vancouver.

Kai-Ji anaripotiwa kuwa na historia ya matatizo ya kiakili na kutokana na hilo amewahi kutagusana na polisi awali. Alifikishwa mahakamani na anasalia korokoroni kulingana na ripoti ya polisi ya jana jioni.

Waliouawa kwenye mkasa huo wana umri wa kati ya miaka mitano na 65 kulingana na Polisi ambao wamesema pia kwamba watu wengi walijeruhiwa wengine vinaya wengine kidogo na wengine hata hawajatambuliwa.

Mashtaka zaidi yanatarajiwa kuongezwa kwenye kesi dhidi ya mshukiwa huyo.

Usimamizi wa jiji la Vancouver ulitangaza kwamba bendera za Canada zitapeperushwa nusu mlingoti kwa muda usiojulikana ili kutoa heshima kwa waathiriwa wa mkasa huo.

Hafla ya Jumamosi ililenga kusherehekea utamaduni na utofauti kuadhimisha siku ya Lapu Lapu, tamasha la kila mwaka linaloandaliwa na watu wa asili ya Ufilipino ambalo pia hutumika kumsherehekea kiongozi aliyepambana na ukoloni wa wahispania.

Share This Article