Mshukiwa mwingine wa mauaji ya Charles Were akamatwa

Tom Mathinji
1 Min Read

Maafisa wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI, wamemkamata mshukiwa mwingine anayehusishwa na mauaji ya mbunge wa Kasipul Charles Ong’ondo Were Aprili 30,2025.

Amos Barasa Kasili, alikamatwa katika eneo la Kibra Darajani baada ya polisi kupokea habari za kijasusi.

Kupitia ukurasa wa X, DCI ilisema kuwa Barasa alikamatwa, baada ya uchunguzi kubainisha kuwa alikuwa mahala pa mauaji hayo, maafisa hao wakisema kuwa alikuwa akiendesha pikipiki iliyokuwa ilimfuata mbunge huyo.

“Ilibainika kuwa Barasa alikuwa akiendesha pikipiki yenye nambari za usajili KMFZ 413W, iliyotumika kumfuata mbunge huyo na baadaye ikatumika kutoroka katika eneo la mkasa baada ya mauaji hayo,” ilisema DCI.

Kulingana na DCI, Barasa ni mhalifu ambaye hujisingizia kuwa mhudumu wa bodaboda huku akishirikiana na magenge ya wahalifu wakati wa operesheni zake.

Alipohojiwa na maafisa wa polisi, mshukiwa huyo alikiri kuhusika katika shambulizi hilo, alisema alipokea shilingi 50,000 kama sehemu ya malipo yake.

Wakati huo huo, pikipiki iliyonaswa inaambatana na Ile iliyonaswa kwenye kamera za CCTV  karibu na majengo ya bunge.

Barasa anazuiliwa na maafisa wa polisi akisubiri kufikishwa mahakamani.

Share This Article