Maafisa wa polisi kaunti ndogo ya Kirinyaga Mashariki, wamemkamata mshukiwa mkuu wa utekaji nyara wa Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi ya Gatuto Joshua Kerai.
Kerai alitekwa nyara Novemba 4, 2025, katika eneo la Kagumo, kaunti ya Kirinyaga.
Patrick Gacoki Muembe na washirika wake wawili ambao wako mbioni, wanadaiwa kumteka nyara mwalimu huyo wakitumia gari aina ya Toyota Ractis, lenya nambari za usajili KCP 816F.
Kupitia ukurasa wa X, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ilisema kuwa baada ya kutekwa nyara, mwathiriwa huyo alipatikana ndani ya gari hilo katika kituo kimoja cha kuuza petroli mjini Kutus, ambapo aliokolewa na wasamaria wema waliompeleka hospitalini.
Maafisa hao wa usalama kisha walianza uchunguzi ambao uliwaelekeza kwenye maficho ya Muembe mjini Kutus na kufanikisha kumkamata mshukiwa huyo.
Uchunguzi wa maafisa hao umebainisha kuwa Muembe amehusishwa na misururu ya uhalifu ikiwa ni pamoja na wizi wa magari na maduka katika eneo hilo.
Kwa sasa, mshukiwa anazuiliwa katika korokoro za polisi huku msako dhidi ya washirika wake ukiendelea.