Maafisa wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), wamemkamata mshukiwa anayehusishwa na uvamizi na uharibifu wa mali katika hospitali ya kaunti ndogo ya Kitengela wakati wa maandamano ya Saba saba.
Elvis Otieno Owino, alitambuliwa na kamera za CCTV kuwa mmoja wa watu waliotekeleza mashambulizi dhidi ya hospitali hiyo.
Baada ya kukamatwa, Owino aliwaelekeza maafisa hao wa upelelezi nyumbani kwake huko Noonkopir,ambako walipata kofia na jaketi ya rangi ya kijivu anazoaminika kuvalia wakati wa kisa hicho.
Anazuiliwa na polisi uchunguzi ukiendelea, huku makachero wakiwatafuta washukiwa zaidi waliovamia hospitali hiyo.
Kisa hicho kilitokea tarehe Julai 7,2025 jioni wakati kundi la wahuni lilipoishambulia hospitali hiyo.
Wahuni hao walitatiza huduma za matibabu zikiwemo upasuaji uliokuwa ukiendelea wa kumsaidia mwanamke mmoja kujifungua, kuharibu vifaa katika chumba cha upasuaji na kuwasha moto kwenye lango la hospitali hiyo.