Zanzibar imepata pigo kubwa kufuatia kifo cha Msemaji Mkuu wa Serikali, Charles Hillary, aliyefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Hillary aliteuliwa na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali mwaka 2023, na kabla ya hapo, mwaka 2021, alihudumu kama Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais — nafasi muhimu aliyotumia kusimamia na kuratibu mawasiliano rasmi ya serikali.
Kabla ya kujiunga na Serikali ya Zanzibar, Charles Hillary alikuwa mwanahabari mwenye uzoefu mkubwa na alifanya kazi katika vyombo vya habari vya kimataifa na vya ndani, ikiwemo Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na Azam Media, ambako alijijengea heshima kwa umahiri wake wa kiuandishi na uanahabari wa kitaalamu.
Kifo chake kimetangazwa rasmi na Serikali ya Zanzibar, huku viongozi wa kitaifa, wanahabari wenzake, na wananchi wakielezea masikitiko yao na kumkumbuka kama mtumishi wa umma na mwanahabari mwenye maono, aliyetoa mchango mkubwa kwa taifa.
Taarifa zaidi kuhusu ratiba ya mazishi na heshima za mwisho zinatarajiwa kutolewa na serikali.