Kijiji tulivu cha Maguguni katika kaunti ndogo ya Thika Mashariki kinaendelea kushuhudia mageuzi makubwa kufuatia mchango wa shilingi milioni 14 kutoka kwa Rotary International.
Fedha hizo zilielekezwa kwa kituo cha Watoto wenye Nguvu International Orphan Care, na zimefanikisha miradi kadhaa ya maendeleo inayolenga kuboresha usalama wa chakula, uendelevu wa mazingira na kujitegemea kwa jamii.
Chini ya usimamizi wa Rotary Club ya Thika, miradi iliyotekelezwa inajumuisha ujenzi wa kivungulio cha kisasa, usakinishaji wa mfumo kamili wa umwagiliaji pamoja na usanifishaji wa mfumo wa taa kwa kutumia nishati ya jua.
Miradi mingine ni pamoja na usanifishaji wa pampu ya mtoni na ile ya kisima, pamoja na ujenzi wa banda la kufugia nguruwe na kuku.
Miradi hiyo inatarajiwa kuinua maisha ya watu na kutoa mafunzo ya vitendo kwa watoto pamoja na wakazi wa eneo hilo.
Katika hafla ya kuzindua miradi hiyo mwishoni mwa wiki, mkurugenzi mtendaji wa Watoto wenye Nguvu International Orphan Care Elizabeth Gitau, alieleza kuwa miradi hiyo imeleta mabadiliko makubwa kwa kituo cha watoto na jamii kwa ujumla.
Alibainisha kuwa awali, walikuwa wakitumia fedha nyingi kwa gharama za umeme, chakula na maji, lakini tangu kukamilika kwa miradi hiyo, gharama za uendeshaji wa kituo zimepungua kwa kiasi kikubwa.
Mwakilishi wa wadi wa eneo hilo, Joachim Njama, alisifu mradi huo na kuyahimiza mashirika mengine kujitokeza kusaidia maendeleo ya jamii, hasa kwa vijana wasiokuwa na ajira ambao mara nyingi huishia mitaani kutokana na ukosefu wa fursa.
Mary Mbinya, mkazi wa kijiji cha Kitofoto kilicho karibu na kituo hicho na mnufaika wa vifaranga waliodungwa chanjo, alisema msaada huo utasaidia sana yeye na kikundi chake cha wanawake kuanzisha shughuli za kujipatia kipato na kuinua hali zao za kiuchumi.