Mwanamuziki wa Tanzania Mr. Sugu ametoa ushauri kwa tume ya uchaguzi nchini humo kusitisha mchakato ambao ilitangaza wa uchaguzi hadi mabadiliko ya kiuchaguzi yafanyike.
Sugu ambaye jina lake halisi ni Joseph Mbilinyi na ambaye ni Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA, Kanda ya Nyasa, anaonekana kukubaliana na mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho Tundu Lissu.
Mbilinyi aliwahi kuhudumu kama mbunge kati ya mwaka 2010 na 2020 alipowakilisha eneo la Mbeya Mjini. Alianza kazi kama mwanamuziki wa mtindo wa Rap mwaka 1990.
Lissu kwa sasa amezuiliwa akikabiliwa na kesi mbili moja ya uhaini kwa kuchochea wananchi kususia uchaguzi na ya pili ya kuchapisha habari zisizo za ukweli kwa kudai kwamba maafisa wa polisi wanatumiwa kutekeleza udanganyifi wa uchaguzi.
Akizungumza na wanahabari leo Agosti 20,2025, Sugu amesema alifahamu kuhusu shutuma dhidi ya Lissu zinazojumuisha kuongea uwongo kwamba Polisi wameshiriki kuiba kura na anashangaa kwanihayo ni mambo wanayoyashtaki kila siku.
Kulingana naye video husambazwa za kudhibitisha suala hilo lakini akashangaa akisema, “Sasa tukiyasema badala ya kuyajibu au kuyafanyia kazi mnakimbilia kutukamata, mtakamata wangapi?”.
Alihimiza ustaarabu akisema nchi ni ya watu wote na ni lazima mambo yafanyike kwa njia sahihi, akiisisitizia tume ya uchaguzi ikomeshe mchakato wa uchaguzi.
Mbilinyi aliwasiliana na wanahabari kwa njia ya kipekee ambapo hakufichua alilokuwa ila aliwatumia tu Link za video akizungumza.
Haya yanajiri wakati ambapo Tanzania inajiandaa kwa uchaguzi mkuu unaopaswa kufanyika Oktoba 29, 2025.