Katika kijiji cha Kasuku, kaunti ya Nyandarua, mmea wa “Thabai”—maarufu pia kama mpupu au stinging nettle—ambao zamani ulionekana kama magugu, sasa umebadilika na kuwa zao muhimu katika mapambano dhidi ya utapiamlo, umaskini na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mkulima Maina Hinga, kilimo cha thabai kilianza kama urithi kutoka kwa mamake. Leo hii, mmea huo si tu umegeuka kuwa chanzo cha riziki, bali pia ni suluhisho la kiafya kwa familia yake na jamii nzima.
“Nahisi vibaya ninapoona watu wakinyunyizia dawa kuuangamiza, ilhali una manufaa makubwa kiafya,” asema Maina.
Huvuna thabai, hukausha na kuupeleka kwa shirika la kijamii la Copycad ambapo husagwa na kufungashwa kwa matumizi ya binadamu.
“Si kazi ngumu. Naweza kuuza gramu moja kwa shilingi moja,” anaelezea.

Anaongeza kuwa mmea huu una virutubisho vingi, hustahimili ukame, na hutoa mavuno mazuri hata wakati hali ya hewa ni ya changamoto. Katika kipindi cha kiangazi, Maina hutegemea maji ya mto mdogo ili kuhakikisha mazao yake yanastawi. Hata hivyo, changamoto kubwa ni katika msimu wa mvua nyingi ambapo shughuli za ukaushaji huwa ngumu.

Katika kijiji cha Kamukukwa, Mary Wanjira ambaye amekuwa akilima thabai tangu mwaka 2013, anasema mmea huo ulimsaidia sana kumtunza mumewe aliyepatwa na ugonjwa wa baridi yabisi (arthritis), hasa katika mazingira ya baridi ya Nyandarua.
“Tulipoanza kuweka thabai kwenye chai na chakula chake, maumivu yalianza kupungua. Sasa anaweza hata kushiriki kazi za shamba,” aeleza Mary.
Anasema pia kwamba huwalisha ng’ombe waliyojifungua majani haya ya thabai kwa kuwa yana chuma, vitamini na kalsiamu muhimu kwa afya ya mifugo.
Thabai ni miongoni mwa mboga na vyakula vya kiasili ambavyo sasa vinazidi kupewa uzito mkubwa na jamii ya Nyandarua. Wakulima wameanza kufufua mazao ya kienyeji kama vile terere, managu, malenge na mchicha.
Mazao haya huvunwa, hukausha na kisha kusindikwa ili kuongeza muda wa matumizi na kurahisisha usambazaji wake sokoni. Hii imesaidia si tu kuongeza kipato bali pia kuboresha lishe ya kaya, hasa kwa watoto na kina mama.

Shirika la Copycad limekuwa mstari wa mbele kuwasaidia wakulima hawa kuongeza thamani ya mazao yao. Kupitia msaada wa mpango wa CASCADE unaofadhiliwa na shirika la CARE Kenya, Copycad huwapa mafunzo wakulima, vikundi vya kina mama, walimu wa shule za Jumapili na waelimishaji wa awali (ECDE) kuhusu kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi, uhifadhi wa mazingira na usalama wa chakula.
Thomas Ndiritu, Mkurugenzi Mkuu wa Copycad, anasema mfumo huu wa kuongeza thamani umewapa wakulima matumaini mapya. “Baada ya kusindika mboga kama mchicha wa kienyeji, osuga, thabai, malenge na managu, bidhaa hizi hudumu muda mrefu na huwa rahisi kuziuza sokoni,” asema.
Kulingana na takwimu za Afya za Idadi ya Watu Kenya, asilimia 18 ya watoto wa chini ya miaka mitano katika Kaunti ya Nyandarua wamedumaa, asilimia 4 wana uzani mdogo, na asilimia 2 wanakabiliwa na utapiamlo mkali. Takwimu hizi zinamaanisha kuwa karibu watoto 14,200 wameathiriwa na udumavu, 4,200 wana uzani mdogo, na 1,600 wanakabiliwa na utapiamlo mkali — hali ya kushangaza ikizingatiwa kuwa Nyandarua ni maarufu kama ‘mfuko wa chakula’ wa taifa.
Mtaalamu wa lishe Esther Karimi amekuwa mstari wa mbele kuelimisha jamii jinsi ya kupika mboga hizi za kienyeji kwa njia inayohifadhi virutubisho vyote. “Sio tu kuwa na chakula kingi, bali ni muhimu kujua namna ya kukitayarisha ili mwili upate lishe inayohitajika,” anasema.
Kwa upande wake, Patricia Wasunna, Afisa Mawasiliano wa Shirika la Global Alliance for Improved Nutrition (GAIN), anasema kuwa mpango wa CASCADE unashirikiana na Serikali ya Kaunti kuhakikisha kuwa Mpango wa Kaunti wa Lishe (CNAP) unatekelezwa ipasavyo. Mradi huo unalenga hasa wanawake walio katika umri wa kuzaa na watoto wa chini ya miaka mitano.
“Tuna furaha kuona kuwa jamii sasa inachukulia kwa uzito changamoto za mabadiliko ya tabianchi na lishe. Thabai sasa inapatikana mwaka mzima kupitia shughuli za ukaushaji na usindikaji,” anasema.
Wasunna anaongeza kuwa juhudi hizi pia zinalenga kuwaelimisha wananchi kuhusu ushiriki wa umma katika upangaji wa bajeti, ufuatiliaji wa utekelezaji wa sera na kuwahimiza kuwawajibisha viongozi wao.
“Tunahakikisha kuwa jamii inajua haki zao na inashiriki kikamilifu katika mchakato wa maamuzi. Mpango wa CNAP si tu waraka wa serikali, bali ni sera ya wananchi.”
Mbali na thabai, jamii pia imeanza kulima kwa wingi maharagwe aina ya Nyota, ambayo ni maarufu kwa kuwa na madini mengi ya chuma na hupendekezwa kwa mama wanaonyonyesha ili kuboresha afya zao na ya watoto wao.
Kutoka katika mazao ya kienyeji ambayo zamani yalionekana kuwa ya kimaskini, sasa wakulima wa Nyandarua wamegundua kuwa ndani ya majani haya ya kijani kuna suluhisho la afya bora, mapato endelevu na kilimo kinachokabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Katika moyo wa mfuko wa chakula wa Kenya, mazao ya asili kama thabai, managu, terere na malenge sasa yameibuka kuwa silaha mpya katika mapambano ya kuondoa utapiamlo na kukuza jamii zilizo imara kiafya na kiuchumi.