Sherehe za Siku ya Mashujaa za leo katika kaunti ya Kwale zinaangazia mpango wa nyumba za gharama nafuu unaoendeshwa na serikali ya taifa.
Wazo la makazi ya gharama nafuu kwa Wakenya lilijiri kwa mara ya kwanza mwaka 2017, wakati huo Uhuru Kenyatta akiwa Rais na William Ruto akiwa naibu wake.
Mpango huo ulikuwa moja kati ya ajenda nne kuu za serikali wakati huo na lengo lilikuwa kukamilisha nyumba za makazi laki 5 katika kaunti zote 47 kufikia mwaka 2022.
Lakini kufikia mwisho wa mwaka 2022, ni nyumba 13, 529 pekee zilikuwa zimekamilishwa.
Alipochukua uongozi wa taifa, Rais William Ruto aliazimia kuendeleza mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, ambapo ulipatiwa jina la “Boma Yangu”.
Serikali inalenga kukamilisha nyumba laki mbili kila mwaka chini ya mpango huo na hivyo kujenga nyumba milioni moja baada ya miaka mitano.
Vile vile, sheria ilibuniwa ya kuratibu mpango huo na ilipitishwa katika bunge na kutiwa saini kuwa sheria na Rais Machi 19, 2024.
Sheria hiyo inahalalisha makato ya kufadhili ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kwa mishahara ya wafanyakazi wote nchini Kenya wa sekta ya binafsi na wa serikali.
Viongozi kadhaa serikalini wamesifia mpango huo wakisema unatoa nafasi za ajira kwa wengi humu nchini.
Kufikia sasa, kuna nyumba ambazo zimekamilishwa tayari kuuzwa kwa Wakenya kupitia kwa jukwaa la Boma Yangu mtandaoni.