Rais William Ruto amezindua awamu ya pili ya mpango wa kitaifa wa kuwapiga jeki vijana kibiashara (NYOTA) katika kaunti sita zilizopo eneo la North Rift.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo katika uwanja wa Eldoret Sports Club, Rais alisema mpango huo ni moja ya jitihada za serikali za kukuza biashara za vijana kote nchini.
“Mpango huu unahusisha kiwango cha juu cha uwajibikaji na uwazi kwa sababu unahusu juhudi za watu kuanzisha miradi inayobadilisha maisha yao,” alisema Rais Ruto.
Wakati wa mkutano huo, shilingi milioni 250 zilisambaziwa vijana wajasiriamali 9,500 kutoka kaunti za Turkana, West Pokot, Trans Nzoia, Nandi, Uasin Gishu na Elgeyo-Marakwet kupitia simu za mkononi.
Chini ya Mpango wa Nyota wa kutoa mtaji kwa biashara zinazochipukia, kila atakayenufaika mwanzoni atapokea shilingi 22,000 kati ya jumla ya shilingi 50,000 zilizowekwa katika mfuko wao wa simu za mkononi wa NYOTA.
Shilingi 3,000 zaidi ziliwekwa kwenye akaunti zao za akiba kwenye Hazina ya Kitaifa ya Malipo ya Uzeeni, NSSF.
Mpango huo, ambao ni ushirikiano kati ya serikali kuu na Benki ya Dunia, ni wenye thamani ya shilingi bilioni 5 unaokusudia kuwawezesha vijana kiuchumi kote nchini.
Umekusudia kuwasaidia vijana 100,000 huku vijana wasiopungua 70 wakitoka katika kila wadi 1,450 kote nchini.