Chama cha Madaktari wa Mifugo nchini Kenya – KVA tawi la Bonde la Ufa kwa ushirikiano na Serikali ya Kaunti ya Pokot Magharibi wameanzisha zoezi la kutoa chanjo kwa mifugo dhidi ya ugonjwa wa ngozi na kichaa cha mbwa katika eneo la Pokot Kusini.
Elijah Lomuton, Chifu wa eneo la Kapyongen alisema wakazi wa eneo hilo wameripoti visa kadhaa vya kung’atwa na mbwa kutokana na kichaa cha mbwa hali ambayo ilisababisha wakulima watano kupoteza ng’ombe wao.
Chifu huyo alisema kuwa hatua hii ya kuchanja mifugo imejiri wakati mwafaka.
Wakiongozwa na Dkt. Michael Ndonga, Mwenyekiti wa KVA tawi la Bonde la Ufa, alisema kuwa wameanza kampeni ya chanjo kwa kushirikiana na Serikali ya Kaunti ya Pokot Magharibi kuhakikisha kuwa wakulima wanaelimishwa kuhusu namna ya kukabiliana na milipuko ya magonjwa ya mifugo.
Ndonga alisema wakulima wa Pokot Kusini wamepatiwa mafunzo ya jinsi ya kuhakikisha mbwa wao wanapatiwa chanjo ili kudhibiti visa vinavyoongezeka vya kung’atwa na mbwa ambavyo ni hatari kwa binadamu na mifugo.
Aliongeza kuwa wanapoadhimisha Siku ya Kupambana na Kichaa cha Mbwa duniani mwezi huu, bado wakulima wengi hawajachanja wanyama wao wa nyumbani ilhali kichaa cha mbwa ni hatari sana iwapo hakitatibiwa ipasavyo, huku wakulima wakitakiwa kuripoti visa vyovyote vya kichaa cha mbwa.
Chama cha Madaktari wa Mifugo tawi la Bonde la Ufa, kinatarajia kuendelea kushirikiana na wakulima wa maeneo mbalimbali mara kwa mara ili kuhakikisha mazingira yasiyo na magonjwa na ambayo yataboresha bidhaa za mifugo na kuinua uchumi.
Afisa wa Mifugo wa Kaunti Ndogo ya Pokot Kusini, Dkt. Charles Kibet, ambaye alisimamia zoezi hilo katika eneo la Chepkono alisema wanatarajia kuchanja mifugo zaidi ya 60,000 kufuatia kisa kilichoripotiwa cha ugonjwa wa ngozi.
Kibet aliongeza kuwa wanaendelea na kampeni ya kuhamasisha wakazi kuhakikisha mbwa wao wanachanjwa dhidi ya kichaa cha mbwa, akitaja visa ambavyo havijathibitishwa ambapo watu wanaaminika kufariki kutokana na ugonjwa huo pamoja na mifugo kadhaa.
Dkt. Teresia Wangari, mjumbe wa KVA alisema kama chama, ni jukumu lao pia kuhakikisha wakulima wanaelimishwa kuhusu umuhimu wa kununua dawa za mifugo na pembejeo kutoka kwa maduka yaliyoidhinishwa na kutafuta madaktari wa mifugo waliothibitishwa kwa huduma bora za afya ya mifugo.
Baadhi ya wakulima wakiwemo Dorcas Komoltich na Kennedy Yopongiro walisema zoezi la chanjo limefanikiwa na pia mafunzo yaliyotolewa kwa wakulima yamewasaidia sana katika utunzaji wa mifugo yao.
Yopongiro alisema awali mifugo wao walikuwa wanakataliwa na wafanyabiashara kutokana na hofu ya kichaa cha mbwa na sasa wanafurahia mabadiliko hayo ambayo yataimarisha maisha yao.