Ni afueni kwa watoto wengi wanaoishi na ulemavu baada ya kuzinduliwa kwa mpango wa kufadhili masomo yao kote nchini.
Waziri wa Elimu Julius Ogamba aliongoza uzinduzi wa mpango wa INUKA unaofadhiliwa na shirika la KPC Foundation.
Uzinduzi huo ulifanyika katika Taasisi ya Elimu Maalum nchini (KISE) katika hafla ambayo pia ilihudhuriwa na Waziri wa Nishati Opiyo Wandayi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri Ogamba aslisitiza dhamira ya serikali kuelekea elimu jumuishi na yenye usawa kwa wote na kuilimbikizia KPC Foundation sifa sufufu kwa kuwawezesha watoto wanaoishi na ulemavu kupitia elimu.
“Utafiti wa Taifa juu ya Watoto Wanaoishi na Ulemavu na Mahitaji Maalum katika Elimu uliofanywa mwaka 2018 ulikadiria kuwa asilimia 11.4 ya watoto wenye umri wa miaka 3-21 nchini Kenya wanaishi na ulemavu. Asilimia hiyo ni sawa na watoto 2,489,252. Utafiti huo pia ulitambua changamoto mbalimbali ambazo watoto wenye ulemavu wanakumbana nazo katika safari yao ya masomo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa miundombinu wanayoweza kutumia na ukosefu wa mafunzo ya kutosha kwa walimu wanaowafunza,” alisema Waziri Ogamba.
“Licha ya changamoto hizi, serikali bado imekusudia kuhakikisha kwamba hakuna mtoto atakayeachwa nyuma. Mipango kama vile INUKA ni muhimu katika kuziba mapengo haya.”
Mpango wa INUKA hutoa ufadhili wa masomo wa shule za sekondari kwa wanafunzi werevu na maskini wanaoishi na ulemavu kutoka kaunti zote 47 kote nchini.
Wanafunzi wawili huandikishwa kwenye mpango huo katika kila kaunti kila mwaka.
Hadi kufikia sasa, mpango huo umewanufaisha watoto zaidi ya 745 ukigharimu zaidi ya shilingi milioni 120.