Mpango wa DRIVE unaolenga kupunguza hatari, kuhakikisha ushirikishaji na shughuli za kuongeza thamani katika sekta ya mifugo, umetoa shilingi milioni 519 kwa sekta hiyo.
Hatua hiyo imepiga jeki uchumi wa ufugaji katika maenep kame nchini.
Mpango huo ambao ulizinduliwa katika mkutano wa wadau leo asubuhi jijini Nairobi unaonekana kuleta mabadiliko makubwa na ya haraka katika maeneo yaliyokuwa yametengwa awali ambayo sasa ni vituo vya uwekezaji.
Ukiongozwa na shirika la maendeleo la Kenya KDC na kuungwa mkono ba benki ya dunia, mpango wa DRIVE unaboresha biashara ya ufugaji katika kaunti 20 zikiwemo Marsabit, Samburu, Narok na Kajiado.
Fedha hizo zinaimarisha ukuaji katika viwango vyote husika vya thamani katika ufugaji kuanzia lishe, uandaaji wa nyama, uandaaji wa ngozi na biashara kwa kuangazia maendeleo yasiyoathiri tabianchi na yanayoongozwa na jamii.
Mkurugenzi mkuu wa shirika la maendeleo la Kenya KDC Norah Ratemo alisema, “Mpango wa DRIVE unafungua thamani ya muda mrefu kwa kusaidia hasa katika ufadhili.”
Katibu wa uhamasishaji wa uwekezaji Abubakar Hassan kwa upande wake alitaja mpango huo kuwa mwongozo wa kivitendo katika kubadili maeneo kame kutoka kuwa maeneo yanayotegemea usaidizi hadi kuwa maeneo yanayoongoza kiuchumi.
Kwa kuunganisha mikopo ya masharti nafuu, fedha zilizowianishwa na ushirikiano wa kimkakati, mpango huu unasaidia Kenya kutekeleza ajenda ya mageuzi ya kiuchumi kutoka Chini kuelekea Juu, huku ukiunda ajira, kuimarisha uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kulinganisha malengo ya kitaifa na vipaumbele vya mashinani.
Walionufaika walisimulia jindi umeleta mabadiliko, wakisisitiza athari halisi za mpango wa DRIVE.
Kwa msaada endelevu na ushirikiano kati ya sekta mbalimbali, mpango wa DRIVE unathibitisha kuwa kuwekeza katika uchumi wa ufugaji kunawezekana na ni jambo la msingi.