Serikali imeleta mpango nafuu na rahisi wa kulipia ada za halmashauri ya bima ya afya ya jamii SHA ambao unalenga watu waliojiajiri katika sekta zisizo rasmi.
Rais Ruto alifichua haya kwenye hotuba yake wakati wa sherehe za 62 za siku kuu ya Madaraka katika uwanja wa Raila Odinga kaunti ya Homa Bay.
Kulingana naye, mpango huo uliopatiwa jina la “Lipa SHA pole pole” utaruhusu wakenya kulipa ada hizo za kila mwaka kwa awamu kulingana na uwezo wao iwe ni kila siku, kila wiki au kila mwezi.
Kiongozi wa nchi alisema hatua hiyo itahakikisha kwamba familia zinadumisha bima ya afya bila kutatizika kifedha, huku wakikuza uendelevu wa hazina hiyo ya bima ya afya.
Kufikia sasa familia milioni 1.7 za sekta zisizo rasmi zimesajiliwa kwenye bima ya SHA, hatua ambayo ni ya mafanikio makubwa kuwahi kuafikiwa katika sekta hiyo katika muda wa mwaka mmoja nchini Kenya.