Makundi ya dharura yanajizatiti kukabiliana na mioto inayokumba baadhi ya mbuga za wanyamapori hapa nchini.
Kulingana na taarifa kutoka Shirika la Mbuga za Wanyamapori nchini (KWS), maafisa wake wameweza kukabili mioto katika maeneo saba, huku mioto ikiendelea kuteketeza baadhi ya mbuga hizo ikiwemo mbuga ya Nairobi na ile ya Ruma.
Kupitia ukurasa wa X, KWS ilisema uchunguzi umeanzishwa kubaini chanzo cha mioto hiyo, ambayo inashukiwa kuanzishwa na shughuli za binadamu na pia hali ya kiangazi inayoshuhudiwa kwa sasa.
“Huku chanzo cha mioto katika mbuga za wanyamapori za Aberdare, South Island na Mlima Elgon kikiendelea kuchunguzwa, shughuli za binadamu kama vile uvutaji sigara,uvunaji asali, uwashaji wa moto kwa maksudi na hali ya kiangazi huenda zimechangia kuzuka kwa mioto hiyo.
Vifaa vya kukabiliana na mioto kama vile ndege aina ya helikopta na magari ya kuzima moto zimepelekwa kukabiliana na mioto hiyo.
“KWS, Vikosi vya Ulinzi (KDF), wasamaria wema na magari ya kuzima moto, yanaendelea kukabiliana na mioto hiyo,” lilisema shirika la KWS.