Wakazi wa eneo la Bulapesa, mjini Isiolo, waliamkia habari za kusikitisha leo Jumatano baada ya mwanamke na watoto wake wanne kuteteketea hadi kufa kwa moto usiku wa manane katika nyumba yao.
Moto huo ambao ulizuka usiku wa manane uliteketeza nyumba yote, na hakuna mtu yeyote aliyenusurika.
Mali ya thamani isiyojulikana pia iliharibika kabisa.
Taharuki ilianza kutanda miongoni mwa wananchi baada ya kubainika kuwa moto huo haukutokea kwa bahati mbaya, bali ulianzishwa kwa makusudi na mwanamke anayedaiwa kuwa kwenye kisasi cha mapenzi.
Wakazi wenye hasira kali walimtafuta mtuhumiwa, wakamshambulia hadi kumuua, kisha wakachoma nyumba yake.
Takribani mita chache ckutoka hapo, katika makaburi ya Bulapesa, wachimbaji walikuwa wakitayarisha kaburi ambapo miili ya marehemu watano ilizikwa saa chache baadaye.
Abdi Duba, ndugu wa familia hiyo, alisema walijaribu kuzima moto kwa msaada wa majirani lakini moto huo ulikuwa mkubwa mno na hakuna kikosi cha zimamoto kilichofika kusaidia.
Wazee wa kijiji walilazimika kutoa wito wa amani na kutuliza hali ya wasiwasi ambayo ilikuwa imetanda.
Chifu wa eneo hilo, Abdi Dida, alithibitisha tukio hilo na kusema kuwa hatua za haraka zilichukuliwa kuwalinda watoto wa mtuhumiwa waliokuwa shuleni baada ya fununu kuenea kuwa vijana walikuwa na mpango wa kuwadhuru.
Chifu Dida alitoa wito kwa vijana na wananchi kwa jumla kujizuia na kutoa nafasi kwa mamlaka kufanya uchunguzi, ingawa wito huo ulifika kuchelewa – kwa sababu mwili wa mtuhumiwa tayari ulikuwa unateketea kwa moto mita chache kutoka mahali alipokuwa akizungumza na wanahabari.
Mzee wa eneo hilo, Omar Godana, pia alitoa wito wa utulivu na kusema kuwa tukio kama hilo halijawahi kushuhudiwa Isiolo.
Kwa mujibu wa Chifu Dida, watoto walioteketea wote walikuwa na umri kati ya miaka 7 hadi 15.
Miili ya marehemu ilizikwa katika makaburi ya Bulapesa kwa mujibu wa mila na taratibu za Kiislamu.