Moto wateketeza soko kuu Dar es Salaam, Tanzania

Marion Bosire
2 Min Read

Wafanyabiashara wa soko kuu la Kawe lililopo katika mtaa wa Umbwelani, eneo la Kawe Ukwamani, jijini Dar es Salaam nchini Tanzania wanakadiria hasara kufuatia moto mkubwa uliozuka huko usiku wa kuamkia leo Jumatatu.

Wahudumu wa zimamoto na wale wa uokoaji walifika katika eneo la tukio mara baada ya taarifa kutolewa na kuanzisha juhudi za kuudhibiti moto huo ambao chanzo chake bado hakijabainika.

Soko hilo la Kawe linafahamika sana kwa uuzajiwa bidhaa mbalimbali zikiwemo nafaka, mboga, matunda na bidhaa nyingine kupitia maduka ya jumla na rejareja.

Walioshuhudia kisa hicho waliambia wanahabari kwamba moto huo ulizuka dakika chache tu kabla ya saa sita usiku na wananchi walifika kusaidia kuokoa mali kabla ya wahudumu kufika.

Kamanda wa kikosi cha zimamoto katika Wilaya ya Kinondoni, Jacob Chacha alisema kwamba walifanikiwa kuzima moto huo na kwamba uchunguzi utafanyika ili kubaini kiwango cha uharibifu na chanzo.

Chacha alisema pia kwamba soko hilo lilikuwa na wafanyabiashara zaidi ya 900 na asilimia 70 wameathirika na moto huo.

Wafanyabiashara husika walifika katika eneo hilo wengi wakizidiwa na hisia kutokana na hasara kubwa ambayo wamepata kwani wengine hawakufanikiwa kuokoa chochote.

Mmoja kwa jina Suzie aliyezungumza na wanahabari alielezea kwamba duka lake lilikuwa na magunia yapatayo 160 ya nafaka na bidhaa nyingine.

Alifanikiwa kuokoa magunia machache tu na akaongeza kwamba wengine waliofika katika eneo la tukio hawakuwa na nia ya kusaidia bali walifika huko kuiba.

Share This Article