Moses Kuria ajiuzulu serikalini

Moses Kuria aliwahi kuhudumu kama Waziri wa Biashara na Waziri wa Utumishi wa Umma. Hadi akijiuzulu, alikuwa akihudumu kama mshauri wa masuala ya kiuchumi wa Rais William Ruto.

Tom Mathinji
1 Min Read
Moses Kuria ajiuzulu serikalini.

Waziri wa zamani Moses Kuria amejiuzulu serikalini, miaka mitatu baada ya kuhudumu katika serikali ya Rais William Ruto.

Kabla ya kujiuzulu kwake, Kuria alihudumu kama mshauri mkuu wa kiuchumi katika serikali ya Kenya Kwanza kwa muda wa miezi 10.

Kupitia kwa taarifa kwenye ukurasa wake wa X, Kuria alithibitisha kuwa amekutana na Rais William Ruto ambaye alikubali hatua yake ya kujiuzulu.

“Leo jioni, nimekutana na rafiki yangu Rais William Ruto. Rais amekubali uamuzi wangu wa kujiuzulu serikalini,” alisema Kuria kwenye mtandao wa X.

Huku akimshukuru Rsi kwa kumpa fursa ya kuhudumu kwenye serikali yake, Kuria alitaja baadhi ya michango yake katika kufanikisha ajenda ya kuimarisha uchumi kutoka chini hadi juu,  almaarufu BETA.

“Namshukuru Rais Ruto kwa kunipa fursa ya kuhumudu wadhifa wa Waziri wa Biashara, Uwekezaji na Viwanda kwa muda wa miezi 11, Wizara ya Utumishi wa Umma kwa muda wa miezi tisa na Mshauri Mkuu wa Kiuchumi kwa muda wa miezi 10,”aliongeza Kuria.

Alisema anapoelekea kutekeleza maswala yake ya kibinafsi, anajivunia kazi aliyoifanya pamoja na Rais Ruto ya kutekeleza mpango wa BETA, alioukarabati kwa ushirikiano na Rais wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Share This Article