Morocco ndiyo timu ya kwanza ya Afrika,kufuzu kwa fainali za kombe la dunia mwaka ujao baada ya kusajili ushindi wa mabao 5-0, dhidi ya Niger, katika mchuano wa kundi E uliosakatwa jana usiku jijini Rabat.
Atlas Lions walionyesha azma yao kutoka kipenga cha kwanza wakicheza mbele ya mashabiki 68,500 waliomiminika katika uwanja uliokarabatiwa upya wa Prince Moulay Abdellah, wakichukua uongozi wa mabao 2-0 kufikia mwishoni mwa kipindi cha kwanza yaliyopachikwa na Ismael Sabiri.
Niger waliocheza wakiwa wachezaji 10 kwa takriban dakika 70 Abdoul-Latif Goume kupigwa kadi ya pili ya njano, walijipata mashakani katika dakika tano za mwanzoni mwa kipindi cha pili Yakoub Elkaabi akiongeza bao la tatu kwa wenyeji.
Mshambulizi wa klabu ya Lille Hamza Igamane aliongeza goli la nne dakika ya 69, kabla ya kutoa pasi kwa Azzedine Ounahi aliyepachika la tano mwishoni mwa mechi kuhitimisha ushindi huo maridhawa.
Ushindi huo unawaeka Morocco uongozini mwa kundi hilo kwa alama 18 ,wakijikatia tiketi kushiriki kipute cha kombe la dunia mwaka ujao katika mataifa ya Marekani,Canada na Mexico kwa mara ya sita.
Mchuano huo ulikuwa wa kwanza kuchezewa katika uwanja wa Prince Moulay Abdellah ambao utaandaa fainali za kombe la mataifa ya Afrika AFCON, ikiwemo mechi ya ufunguzi ya kundi A kati ya Morocco na Comoros Disemba 21 na fainali ya Januari 18 mwaka ujao.