Mkuu wa zamani wa shirikisho la soka Afrika ya Kati afungwa jela

Tom Mathinji
2 Min Read
Mkuu wa zamani wa shirikisho la soka la Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Patrice-Edouard Ngaïssona

Mkuu wa zamani wa shirikisho la soka la Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Patrice-Edouard Ngaïssona, amepatikana na hatia 28 ya  uhalifu wa kivita dhidi ya binadamu.

Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), walimshtaki Ngaïssona pamoja na Alfred Yekatom, kwa kuratibu mashambulizi dhidi ya idadi ya Waislamu nchini humo mwaka 2013-14.

Yekatom alipatikana na hatia ya mashtaka 20. Majaji hao walitoa uamuzi wao baada ya kesi iliyodumu kwa takriban miaka minne iliyohusisha mashahidi zaidi ya 170 na karibu vipengele 20,000 vya ushahidi.

Ngaïssona alihukumiwa miaka 12 na Yekatom miaka 15.

Ghasia zimeikumba CAR kwa muda mrefu wa muongo mmoja uliopita, lakini makubaliano ya hivi majuzi ya amani yalisababisha kuvunjika kwa makundi mawili ya waasi mwezi huu.

CAR ilitumbukia katika machafuko mwaka wa 2013 wakati waasi wengi wa Kiislamu kutoka kundi la Séleka waliponyakua mamlaka katika nchi hiyo yenye Wakristo wengi.

Kundi la wanamgambo wengi wa Kikristo, wanaoitwa anti-Balaka, walisimama kukabiliana na Séleka baada ya Rais wa wakati huo François Bozizé kuondolewa madarakani.

Ngaïssona na Yekatom walitiwa hatiani kwa makosa mengi ya uhalifu, yakiwemo mauaji, mateso na kutesa kundi la kidini.

Mwendesha mashtaka aliweka madai ya mfumo wa amri, akisema Ngaïssona alitoa pesa na maagizo kwa vikundi vya anti-Balaka mnamo 2013 na 2014.

Share This Article